Hali ya wasiwasi imetanda kaskazini mwa Uganda baada ya ugonjwa wa kusinzia japo sio malale kuwauwa takriban watu laki mbili. Wizara ya afya nchini Uganda inasema takriban watu elfu nne wameathiriwa na ugonjwa huu. Ni ugonjwa uliozusha hofu miongoni mwa watu kwa sababu chanzo chake hakijulikani na hawajui wajikinge vipi. Maafisa wa wizara ya afya na wabunge wa kutoka la Acholi ambalo ndilo limeathirika zaidi na ugonjwa huu, kuanzia Alhamis wamekuwa wakizuru wilaya za Kitgum, Lamwo na Pader ambazo zina kesi nyingi sana ya watu wanaougua ugonjwa huo wa kusinzia. Wilaya hizi ziko karibu na mpaka wa Sudan. Itakumbukwa kuwa kesi za kwanza za ugonjwa huu ziligunduliwa nchini Sudan miaka ya themanini. Dr. Issa Makumbi kamishna anayehusika na magonjwa ya maambukizi kwenye wizara ya afya ni miongoni mwa maafisa wa afya wanaolizuru eneo lililoathirika. Akizungumza na sauti ya Amerika kwa njia ya simu kutoka wilayani Kitgum Dr. Makumbi alisema waathiriwa mara kwa mara huanguka kama watu wanaougua kifafa. Anasema pia kuwa wana ishara za watu wanaougua ugonjwa wa utapia mlo kwa sababu hawali vizuri. Watoto walio kati ya miaka miwili na kumi na tano ndio wanaoathirika zaidi na ugonjwa huu. Haijabainika wazi ugonjwa huu wa kusinizia unasambazwa vipi au unaambuka vipi na kwa hivyo ni vigumu kujikinga. Kisa cha kwanza cha Ugonjwa wa kusinzia kiliripotiwa nchini Uganda mwaka wa 2009. Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, utafiti kuhusu chanzo cha ugonjwa huu umekuwa ukifanyika nchini Uganda na Marekani. Aidha daktari Makumbi anasema zaidi ya wanafunzi elfu moja mia tano wameacha kwenda shuleni kutokana na ugonjwa huu. Kufikia sasa, wizara ya afya haijatoa mikakati yoyote ya kukabiliana na ugonjwa huu wa kusinzia kwa sababu ugonjwa huu ungali ni kitendawili ambacho bado hakijateguliwa.
Maelfu ya watoto wamekufa nchini Uganda tangu mwaka wa 2009