Hii ni baada ya oparesheni ya kijeshi dhidi ya kundi hilo iliyotekelezwa leo na vikosi cya Uganda, Sudan kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati dhidi ya LRA.
Kulingana na naibu wa msemaji wa jeshi la Uganda UPDF, Kanali Deo Akiiki, kikosi cha wanajeshi wa Uganda UPDF, Sudan Kusini SSPDF na wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wametekeleza operesheni maalum ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuharibu kambi tatu za kundi la waasi la Lords Resistnce Army LRA.
Operesheni imefanyika mashariki mwa mji wa Sam Oundja, Huate Kotto, karibu na mpaka na Sudan. Kambi zote zimeharibiwa na silaha kadhaa kupatikana.
Uganda inasema kwamba kundi la LRA bado ni hatari kwa usalama wa nchi za Maziwa Makuu.
Hakuna taarifa za uhakika mahali alipo kamanda mkuu wa LRA Joseph Kony lakini makamanda wake wanakabiliwa na mashtaka katika mahakama mbalimbali duniani ikiwemo Dominic Ongwen aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 na mahakama ya ICC, na anazuiliwa gerezani nchini Norway.
Kamanda mwingine Thomas Kweyelo, wiki iliyopita alipatikana na kesi 44 za kujibu katika mahakama ya Uganda kuhusiana na ukandamizaji wa haki za binadamu, unajisi, mauaji, kuandikisha watoto katika jeshi, kuharibu kambi za wakimbizi, miongoni mwa mengine.
Kundi la LRA lilianzia kaskazini mwa Uganda ambapo lilitekeleza mauji, unajisi na dhuluma nyingine za kibinadamu.
Joseph Kony na kamanda wake Vincent Otti, wanatafutwa na mahakama ya ICC.
Serikali ya Marekani ilitangaza tuzo ya dola milioni 5 mnamo mwaka 2021 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamwatwa kwa Joseph Kony, kamanda mkuu wa LRA.