Uganda yaombwa kuheshimu upinzani.

Viongozi wa vyama vya upinzani wakiongozwa na Dkt Kizza Besigye (hushoto).

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limeitaka mamlaka ya Uganda kuacha kuvuruga mikutano ya amani ya kisiasa nchini humo hasa kwa kutumia gesi ya kutoa machozi, likisema kuwa vitendo hivyo vinakiuka haki ya watu kukusanyika kwa uhuru na kujieleza.

Uganda inatarajiwa kuitisha uchaguzi wa rais mwaka ujao huku kampeni zikipangwa kuanza Novemba tisa. Waganda wamelalamikia matumizi ya nguvu ya mara kwa mara yanayofanywa na polisi kuzuia viongozi wa upinzani kuhutubu kwenye mikutano au hata kukutana na wafuasi wao.

Wiki iliyopita, kiongozi mkuu wa upinzani Kizza Besigye alimshutumu rais Yoweri Museveni kwa kuchochea ghasia dhidi ya wapinzani wake. Hiyo ni pamoja na tukio ambalo polisi walimvua nguo mwanamke aliyekuwa kwenye msafara wake na kumtupa nyuma ya gari lililokuwa wazi.