Uganda: Mwandishi Kakwenza aliteswa, ripoti ya gereza yaeleza

Mwandishi wa vitabu wa Uganda Kakwenza Rukirabashaija (Twitter/@KakwenzaRukira)

Ripoti ya matibabu iliyotolewa na idara ya magereza nchini Uganda, inaeleza kwamba mwandishi wa vitabu, Kwakenza Rukirabashaija, alikuwa na alama za mateso kabla ya kufikishwa gerezani.

Mwandishi huyo yuko rumande katika gereza la Kitalya, kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii na kutuma ujumbe wa Twitter wenye matusi na dharau dhidi ya mwanaye rais wa nchi hiyo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, pamoja na Rais Yoweri Museveni mwenyewe.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba mshukiwa huyo alikuwa na makovu katika sehemu mbalimbali za mwili, na kwamba alikuwa akitumia dawa za kutibu majeraha.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, ripoti hiyo ya magereza inajiri siku mbili tu baada ya maafisa wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Uganda (UHRC) kumtembelea Kakwenza gerezani na baadaye kutuma ujumbe wa twitter kuelezea kuhusu hali yake, wakisema kwamba alikuwa na makovu na majertaha mwilini mwake.

Kakwenza alichukuliwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama kutoka nyumbani kwake Kisaasi, kitongoji cha Kampala, mnamo Desemba 28, mwaka jana, na baadaye kushikiliwa mahali pasipojulikana, ambapo alidaiwa kuteswa.