Rais wa Uganda, Yoweri Museveni anasema yupo tayari kuachia madaraka iwapo atashindwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Februari 18.
Bwana Museveni amekuwa mwepesi kuelezea kwamba ana imani kubwa kwa vyovyote vile hawezi kupoteza katika kinyanga’nyiro hicho.
Rais ambaye anawania kiti hicho kwa tiketi cha tawala cha NRM amesema ana mambo mengi ya kufanya hata akiondoka kwenye siasa hivi leo.
Alizungumza hayo Jumapili katika mkutano na waandishi wa habari ambao ulifanyika kwenye ikulu ya rais mjini Kampala. Alipoulizwa kama ana mipango ya kuandaa mrithi wake katika wadhifa huo wa urais, bwana Museveni amesema kuwa Uganda siyo shamba lake la ndizi na hivyo hawezi kuandaa mrithi.
Your browser doesn’t support HTML5
Lakini wakati fulani katika mkutano mmoja wa kampeni bwana Museveni aliwahi kusema kuwa Uganda ni shamba lake la ndizi na hawezi kumuachia mtu yoyote kuvuna ndizi zake.
Bwana Museveni ambaye ana umri wa miaka 71 katika uchaguzi huu anakabiliwa na ushindani mkali dhidi ya wagombea wawili wakuu wa upinzani, Dr. Kiiza Besigye wa chama FDC na bwana Amama Mbabazi , waziri mkuu wa zamani ambaye anawania urais kama mgombea huru.