Wizara ya afya nchini Uganda imethibitisha kwamba mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano amepimwa na kupatikana na virusi vya Ebola ikiwa ni mara ya kwanza kwa virusi hivyo kuenea kuvuka mipaka ya kitaifa wakati wa kile ambacho kinaonekana kuwa mlipuko wa pili mkubwa kutokea katika historia ya ugonjwa huo.
Mtoto huyo raia wa kongo aliwasili Uganda siku ya Jumapili na familia yake na amewekwa katika eneo maalum ndani ya hospitali mjini Kasese iliyopo kwenye mpaka wa magharibi wa Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo-DRC.
Habari hizo ni pigo kwa wafanyakazi wa afya Kongo ambao wamekuwa kwa miezi kadhaa wakipambana kuzuia kusambaa kwa virusi vya Ebola kutoka nchini Kongo ambako kuna zaidi ya watu 2,000 waliorodheshwa kuwa wameambukizwa virusi hivyo katika muda wa miezi 10 iliyopita na takribani watu 1,400 kati yao wamefariki.
Wizara ya afya na shirika la afya dunia wameshapeleka timu ya dharura hadi Kasese kuwapima watu wengine ambao huwenda wako katika hatari ya kuambukizwa na kufuatilia kwa karibu matukio katika mji huo.