Ufalme wa Buganda hatimaye umempata mrithi

  • Sunday Shomari

Kabaka Ronald Mutebi, mfalme wa Buganda, mmoja kati ya wafalme wanne wa kijadi nchini Uganda.

Ufalme wa Buganda umepata mrithi aliyezaliwa mwezi wa saba mwaka uliopita, lakini mtoto huyu amezaliwa nje ya ndoa yake na kupelekea mawazo mbali mbali kutoka kwa Waganda.

Ufalme wa Buganda hatimaye umempata mrithi atakae weza kuchukua nafasi wa mfalme wa hivi sasa Kabaka Ronald Mutebi. Mwana mfalme mrithi Richard Ssemakokiro alizaliwa mwezi wa saba mwaka uliopita lakini habari za kuzaliwa kwa mtoto huyu zilitangazwa Jumanne jioni na waziri mkuu wa ufalme wa Buganda JB Walusimbi.

Kufikia sasa, mama ya mtoto huyu hajulikani lakini waganda wanasema kilicho muhimu kwao ni kumpata mrithi na hawajali nani kamzaa mrithi huyu.

Habari za kuzaliwa kwa mwana mfalme Richard zimewafurahisha waganda wengi. Kwani kufikia sasa, ufalme wa Buganda umekuwa ukisubiri kwa hamu kuona ni nani atakayemrithi mfalme Kabaka.

Ingawa Kabaka alikuwa na kijana aliyemzaa na mama mnyarwanda kabla ya kufunga ndoa, kulingana na mila na tamaduni za Buganda kijana huyu hawezi kuwa mrithi kwa sababu mamake si Mganda.

Mfalme au Kabaka Ronald Mwenda Mutebi wa pili mwenye umri wa miaka 56 alifunga ndoa kwenye kanisa la Anglikana na Bi.Sylvia Naginda Luswata mwaka wa 1999. Ndoa yao ilibarikiwa na mtoto mmoja wa kike.

Tukitilia maanani kuwa Kabaka alifunga ndoa kanisani na kulingana na mafunzo ya Bibilia hafai kuwapata watoto nje ya ndoa, baadhi ya waganda walisema hawana tatizo na jambo hilo. Mkazi mmoja ameiambia VOA kwamba "hakuna shida hapo kwa sababu wafalme waliomtangulia walikuwa na wanawake ishirini, thelathini kwa hivyo hakuna shida kabaka kuzaa na mwanamke mwingine".

Hata hivyo kunao waganda ambao hawajafurahishwa na jinsi utamaduni wa Buganda unavyomteua mrithi.

Siraji mkazi wa Kampala anasema kuna hali ya kutatanisha kwani kabaka tayari ana mtoto wa kiume na pili kaowa mke wa ndoa.

“Huyo mke wa ndoa kazaa mtoto, mtoto ni binti, sasa kwani binti si binadamu, yeye hawezi kuwa malkia, mbona Uingereza kuna malkia! Inakuaje mtu azae mtoto ambaye si wa ndoa, na wewe unasema ni Mfalme? Ikiwa hathamini dini na maadili mbona ndoa yake kaifanya ndani ya kanisa.”

Kabaka Mwenda Mutebi ni mfalme wa 36 wa Buganda.