Obama Akanusha Ameamrisha Simu za Trump Kusikilizwa

Rais Barack Obama

Uongozi wa Rais Donald Trump bado haujatoa tamko kujibu kauli ya msemaji wa Rais mstaafu Barack Obama ikikanusha kwamba aliamrisha kusikilizwa kwa siri mawasiliano ya simu ya Trump wakati wa kampeni kabla ya uchaguzi wa Marekani, mwaka jana.

Msemaji wa Obama ametoa tamko baada ya Trump kuandika mlolongo wa ujumbe wa tweets Jumamosi asubuhi akidai kwamba Obama “ aliamuru simu zake zirikodiwe kwa siri katika jengo la Trump” mjini New York kabla ya uchaguzi.

Msemaji wa Obama amesema kwamba madai ya Trump yalikuwa “ kwa kifupi sikweli.”

Trump hakueleza chanzo cha madai yake, au kutoa ushahidi wowote kwamba kulikuwa na uthibitisho wowote wa kielektronikia, lakini akafananisha na kusikilizwa kwa siri simu zake kama wakati wa kashfa ya Watergate iliyopelekea hatimaye mwaka 1974 Rais wa zamani wa Marekani Richard Nixon kujiuzulu.

Kashfa hiyo ilianza na mlolongo wa “vitimbi vya kisiasa” vilivyokusudiwa dhidi ya chama cha demokratik ikiwa ni njama ya wafuasi wa Nixon, na ikachukua sura mpya baada ya maafisa wa White House kutoboa siri kuwa Nixon aliruhusu operesheni hiyo ya kufuatilia mazungumzo ya chama cha Demokratik ifanyike White House, na kurikodi mazungumzo ya simu zao nyingi.

Lakini hakuna afisa yoyote wa White House wakati wa Uongozi wa Obama “ aliyewahi kuingilia uchunguzi wowote ulioendeshwa na wizara ya sheria,” amesema Kevin Lewis, msemaji wa rais mstaafu, akisisitiza kuwa katazo hilo ndio ilikuwa “amri ya msingi” katika utawala wa Obama.

Katika taarifa hiyo, Lewis amesema haikuwa Rais Obama wala afisa yoyote wa White House aliyewahi kuamrisha uchunguzi wa raia yoyote wa Marekani. Kauli yoyote inayopendekeza hilo ni Uongo tu.

VOA imewataka maafisa wa White House kutoa tamko kuhusu tukio hilo la Jumamosi lakini hawakuweza kupata majibu hayo mara moja. Sio Idara ya FBI wala Idara ya Sheria iliyoweza kutoa tamko kuhusiano na madai hayo.