Uchumi wa mashariki ya kati umekuwa chini ya makadirio

Shirika la fedha la kimataifa (IMF) Jumapili limesema uchumi wa mashariki ya kati umekuwa chini ya makadirio ya ukuaji kutokana na kupunguzwa kwa uzalishaji wa mafuta na mzozo wa Israel na Gaza, hata kama mtazamo wa kiuchumi wa kimataifa unaendelea kuwa thabiti.

Licha ya kutokuwa na uhakika, uchumi wa dunia umekuwa wa kustahimili kwa kushangaza, mkurugenzi mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva, aliliambia jukwaa la fedha la waarabu akiwa Dubai, huku akionya juu ya uwezekano wa athari kubwa zaidi katika uchumi wa kikanda kutokana na kuendelea kwa mgogoro wa Gaza.

Katika ripoti ya uchumi wa kikanda ya mwezi uliopita, IMF ilirekebisha utabiri wake wa ukuaji wa pato la taifa kwa mashariki ya kati, na Afrika kaskazini hadi kufikia asilimia 2.9 kwa mwaka huu, ukiwa chini ya makadirio ya Oktoba, kutokana na kupunguzwa kwa uzalishaji wa mafuta kwa muda mfupi, na mzozo wa Gaza.