Uchaguzi wafanyika Mashariki mwa DRC

Masanduku ya kupigia kura DRC

Wapiga kura ambao hawakupata nafasi ya kushiriki uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Januari mwaka huu nchini DRC kwa sababu ya vurugu na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, hususan katika maeneo ya Mashariki mwa nchi hiyo, walipiga kura Jumapili.

Zoezi hilo liliendelea katika miji ya Butembo na Beni, ambako ongezeko la visa vipya vya Ebola imeendelea kuripotiwa, huku kukiendelea kuwa na shutuma mbalimbali kuhusu sababu halisi ya wakazi wa maeneo hayo kutoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa Januari.

Shirika la habari la Associated Press (AP) linaripoti kuwa wapiga kura walionekana wakiosha mikono yao kabla ya kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.

Baadhi ya wakazi waliohojia na AP walisema hawaamini kuwa Ebola ndiyo ilisababisha wasishiriki upigaji kura wa mwezi Januari, na kwamba zilikuwa ni njama za watu waliotaka kujifaidi kisiasa.

Ingawa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umeripotiwa katika mji wa Butembo, utafiti uliofanywa na jarida la Lancet Infectious Disease Journal wiki iliyopita unaonyesha kuwa mmoja kati ya watu wanne anaamini kuwa Ebola ni ugonjwa wa kubuniwa.