Tume ya uchaguzi ya kitaifa ya Somaliland ilisema kuwa zoezi hilo lilifungwa saa 12 za jioni kwenye vituo 2,000 vya kupigia kura. Zaidi ya wapiga kura milioni moja walikuwa wamejiandikisha kupiga kura, wakati shughuli za kuhesabu kura zikianza mara moja baada ya vituo kufungwa, tume ya uchaguzi imeongeza kusema.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Muse Hassan, alisema kuwa kura zilianza kuhesabiwa kwenye vituo, halafu kwenye wilaya na hatimaye kwenye majimbo kabla ya matokeo kutangazwa. Alisema kuwa matangazo yatafanywa kufikia Novemba 21. Mkuu wa polisi wa Somaliland Jenerali Mohamed Adan Saqadhi alisema kuwa zoezi hilo liliendelea kwa njia ya amani kote kwenye eneo hilo.
Wagombewa watatu akiwemo rais wa sasa Muse Bihi Abdi walikuwa wakiwania kwenye uchaguzi huo. Kwenye mahojiano na VOA Idhaa ya Kisomali, wagombea wote watatu waliahidi kuimarisha demokrasia, uchumi na kushinikiza kutambuliwa kimataifa. Somaliland imekuwa ikiomba kutambuliwa kimataifa kwa miaka 33.