Uchaguzi huo wa awali umetajwa na wachambuzi wa kisiasa kama ni kigezo muhimu kwa mstakabali wa muungano huo wa kisiasa. Uchaguzi mkuu nchini Kenya unatarajiwa kufanyika tarehe nane mwezi Agosti
Profesa Hermnan Manyora, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya, ameiambia Sauti ya Amerika kuwa kukosa kufanya uchaguzi wa awali ni kinyume na maadili ya kidemokrasia.
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), moja ya vyama vikubwa vya upinzani nchini Kenya, kimeahirisha uchaguzi wake katika baadhi ya maeneo, huku wanachama wakilalamika kuwa uligubikwa na dosari na kwamba majina ya baadhi ya wagombea hayakuwapo kwenye makaratasi ya kupigia kura.
Uchaguzi huo uliohairishwa utaendelea tena baada ya wiki moja, kwa mujibu wa maafisa wa chama hicho.
Robert Arunga, mwanachama wa bodi ya ODM ameiambia Sauti ya Amerika licha ya matatizo ya hapa na pale, uchaguzi huo uliendelea. "Hili ni zoezi kubwa na makosa madogo madogo hayawezi kukosekana," alisema Arunga.
Vyama vingine vinavyofanya chaguzi za awali ni pamoja na kile cha Wiper Democratic Movement, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC).
Viongozi wa upinzani nchini Kenya, chini ya Muungano wa kitaifa wa National Super Alliance (NASA), wanatarajiwa kutangaza yule atakayepeperusha bendera yao wakati wowote sasa, kufuatia mikutano mingi ambayo imekuwa ikifanyika kwenye miji mbali mbali.
Chama cha Jubilee kinatarajiwa kuanza uchaguzi wake wa mchujo siku ya Ijumaa.