Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umethibitisha kuuwawa kwa wanadiplomasia wake watano kwenye shambulizi la bomu la Jumanne katika mji wa kusini mwa Afghanistan wa Kandahar.
Maafisa wa serikali wamesema kuwa shambulizi hilo liliuwa watu 11 na kujeruhi wengine 16 wengi wao wakiwa maafisa wa serikali ya Afghanistan.
Gavana wa jimbo hilo, Homayun Aziz pamoja na balozi wa UAE mjini Kabul, Juma Mohammed Abdullah al Kaabi ni miongoni mwa waliojeruhiwa.
Wizara ya mambo ya nje ya UAE imesema kuwa balozi huyo aliitembelea Kandahar kwa ziara ya huduma za dharura yenye lengo la kuwasaidia yatima na pia kutoa misaada ya elimu.
Kundi la kigaidi la Taliban limekana kuhusika na shambulizi hilo na badala yake kulaumu uhasimu miongoni mwa vikundi vya jimbo hilo.