Meli hiyo iliyokuwa inatokea Equatorial Guinea ikielekea Malta ilizama Ijumaa na jeshi la majini la Tunisia liliwaokoa mabaharia wote saba wa meli hiyo.
Meli hiyo ilikuwa imebeba kati ya tani 750 na elfu moja za mafuta na ilituma ujumbe wa hatari ikiwa maili saba kutoka Gabes ambapo jeshi la majini la Tunisia lilifuatilia, maafisa walisema.
Wizara ya ulinzi ilisema katika taarifa yake iliyopelekwa kwa Reuters kuwa kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira jeshi la majini la Tunisia litafanya kazi na nchi ambazo zimeeleza nia yao ya kusaidia.
Vyombo vya ndani vya habari vimesema Italia ilikuwa imejitolea kusaidia na inatarajiwa kupeleka meli za jeshi zilizobobea katika kushughulikia maafa ya baharini.
Siku ya Jumamosi, Maafisa wa Tunisia walianzisha uchunguzi kufuatia kuzama kwa meli hiyo, ambapo wizara ya mazingira ilisema ilisababishwa na hali mbaya ya hewa.
Ilisema kutawekwa vizuizi kuzuia kusambaa kwa mafuta na kuitenga meli hiyo iliyozama kabla ya kuanza kunyonya mafuta yaliyomwagika baharini.
Pwani ya mji wa kusini wa Gabes imekabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa miaka mingi, huku taasisi za mazingira zikisema viwanda katika eneo hilo vimekuwa vikitupa uchafu moja kwa moja baharini.
Chanzo cha habari hizi ni shirika la habari la Reuters