Chadema yampendekeza Tundu Lissu 2020

Tundu Lissu

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimempendekeza Jumatatu mwanasiasa machachari, Tundu Lissu kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020, akichuana na Rais John Magufuli anayewania muhula wake wa pili.

Lissu alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 405 sawa na asilimia 91.7 za wapiga kura katika baraza kuu la chama hicho katika ukumbi wa mlimani City jijini Dar es salaam.

Tundu Lissu alipambana na wagombea wengine wa chama hicho waziri wa zamani wa utalii Lazaro Nyalandu aliyejiunga na chama hicho kutoka chama tawala cha CCM na Dkn MayRose Majinge.

Lissu alifuatiwa na Lazaro Nyalandu aliyepata kura 36 sawa na asilimia 8.14 na Dr Mayrose Majige aliyepata kura 1 sawa na asilimia 0.23.

Mgombea huyo atathibitishwa rasmi Jumanne katika mkutano mkuu wa chama hicho.

Jumla ya wajumbe 442 walipiga kura hizo na hakuna iliyoharbika kwa mujibu wa katibu mku wa chama hicho ndugu John Mnyika.

Wakati huohuo Baraza Kuu la Chadema limempitisha Salum Mwalimu kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Said Issa Mohammed pia amepitishwa na baraza hilo kuwa mgombea wa urais wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Sunday Shomari, Washington, DC.