Tume ya uchaguzi Uganda yapiga marufuku mikusanyiko ya watu katika kampeni

Bobi Wine - mgombea urais Uganda 2021

Tume ya uchaguzi nchini Uganda imepiga marufuku mikusanyiko ya watu wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao 2021.

Marufuku hiyo imetolewa siku moja baada ya rais Yoweri Museveni kusema kwamba wagombea wenzake wanakusanya watu licha ya kuwepo janga la virusi vya Corona, watachukuliwa hatua haki.

Taarifa ya tume ya mwenyekiti wa tume uchaguzi Jaji Simon Byabakama kwa vyombo vya habari, imesema kwamba “tume imeshuhudia baadhi ya wagombea wa viti mbalimbali wakiwemo wa urais wakifanya mikutano mikubwa ya kampeni kinyume na maelekezo ya tume.”

Mgombea wa urais Robert Kyagulanyi,maarufu Bobi Wine, amekuwa akiandaa mikutano mikubwa ya kampeni. Umati mkubwa wa wafuasi umekuwa ukijitokeza kumlaki barabarani, mijini na katika viwanja vya michezo kwa ajili ya kampeni, kaskazini mwa Uganda.

Rais Yoweri Museveni ambaye anagombea muhula wa sita madarakani, kwa upande wake amekuwa akikutana na baadhi ya wanachama wa chama chake cha National Resistance Movement, huku mikutano yake ikipeperushwa na vyombo vyote vya habari katika sehemu anazokwenda, pamoja na televisheni ya taifa – UBC.

Wagombea wengine kama Jenerali Mugisha Muntu na Generali Henry Tumukunde, nao wamekuwa wakiandaa mikutano na wafuasi wao japo imekuwa ikihudhuriwa na watu wachache.

Polisi wakamata wafuasi wa Bobi Wine

Saa chache baada ya tume ya uchaguzi kutoa taarifa yake, polisi katika wilaya ya Oyam, kaskazini mwa Uganda, wamemkamata naibu mwenyekiti wa chama cha National Unity Platform (NUP), cha Bobi Wine.

Dr. Lina Zedriga amekamatwa pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho kwa kubeba watu wengi kwenye gari lake.

Bobi Wine anafanya kampeni kaskazini mwa Uganda na amekuwa wilayani Oyam, Apac na Lira, leo alhamisi, ambapo idadi kubwa ya watu walijitokeza kumlaki na kuathiri shughuli za biashara na usafiri eneo hilo. Polisi walijaribu kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Bobi Wine waliokuwa wakiimba na kusherehekea barabarani, bila mafanikio.

Waliokamatwa wanazuliwa katika kituo cha polisi cha Lolo.

“Sina shaka kwamba tutashinda uchaguzi huu. Ninachowaomba ni kwamba mjitokeze kwa wingi na mpige kura. Linda kura yako. Salia katika kituo cha kupiga kura baada ya kupiga kura yako. Subiri hadi wamalize kuhesabu.” Bobi Wine ameambia wafuasi wake wilayani Apac.

Polisi watumiwa gesi ya kutoa machozi dhidi ya wafuasi wa upinzani

Wagombea wa urais kupitia vyama vya upinzani kama Patrick Amuriat Oboi wa chama cha Forum for Democratic Change – FDC, na Luteni Jenerali Henry Tumukunde anayewania kama mgombea huru, nao wameshuhudia visa vya polisi kutawanya mikutano yao kwa kutumia gesi y akutoa machozi.

Tume ya uchaguzi inataka kila mgombea kuhakikisha kwamba mikutano yao haizidi watu 70 japo wizara ya afya imesema kwamba watu 200 wanaweza kuhudhuria mikutano hiyo kutokana na janga la virusi vya Corona.

Museveni afanya kampeni kwa njia ya radio, runinga na facebook

Rais Yoweri Museveni ameendelea kufanya kampeni zake kwa njia anayoita ya kisayansi, akiwaahidi raia wa Uganda maisha mema katika siku zijazo.

Shirika la habari la serikali UBC na radio zake zote zinazotangaza kwa lugha za kiasili zinapeperusha kampeni za rais Museveni, sawa na kuonyeshwa kwenye ukurasa wake wa facebook.

Wapinzani wanadai kwamba shirika la habari la serikali limekataa kuonyesha mikutano yao moja kwa moja ilivyo na mikutano ya Museveni, na kwamba ni gharama ghali kulipia katika vituo vya habari vya kibinafsi.

Ushuru wa kila siku uliowekewa mitandao ya kijamii imewafanya raia wengi wa Uganda kutuingia katika mitandao ya kijamii na kutazama video za moja kwa moja za wanasiasa wanapofanya kampeni.

Umri wa Museveni wazua mdajala

Swala la umri wa Museveni, ambaye ana miaka 76 linaendelea kuzua mjadala mkali, wapinzani wake wakisema kwamba katika mazingira ya Afrika, umri wake hamruhusu kuendelea kugombea mhula mwingine madarakani na badala yake wanamtaka awe mshauri katika maswala ya uongozi.

Lakini akihutubia wafuasi wake alhamisi, Museveni ametaja mjadala huo kuwa “upuuzi.”

Amesema kwamba “uongozi sio biolojia ambapo unaweza kuzungumzia vijana na wazee. Tunazungumzia kuhusu nani aliye na fikra na mawazo ya kuongoza nchi. Kwa mfano, mimi ni mkristo. Mafundisho ya kikirsto yamezeeka sana. Je, tuachane na mafundisho hayo kwa sababu walioyatoa walizeeka na kuondoka miaka 4000 iliyopita?” ameuliza Museveni akiwa katika uwanja wa chuo kikuu cha Muni, mjini Arua katika kampeni yake ya kisayansi ambapo alikutana na wagombea wa chama cha NRM na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa chama hicho.

Uchaguzi mkuu wa Uganda utafanyika Januari 14 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC