Tume ya Uchaguzi Kenya ina wasiwasi wa kufikia malengo yake

Rais Uhuru Kenyatta atembelea kituo cha kuandikisha wapiga kura mjini Embu

Wiki moja kabla ya kumalizika zoezi la Wakenya kujisajili ili waweze kupiga kura kuna dalili kuwa Tume ya Uchaguzi nchini humo haitaweza kufikia malengo yake ya kuwafikia wananchi takriban milioni sita.

Kwa mujibu wa Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA maeneo mengi nchini humo yameripotiwa kusajili idadi ndogo ya wapiga kura wakati kunaripoti kuwa maeneo megine yamesusia zoezi hilo.

Takwimu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi (IEBC) nchini Jumatatu, zinaonyesha Wakenya wachache wanaendelea kujitokeza kujisajili kupiga kura.

Mwandishi wetu anaongeza kuwa hata baada ya wanasiasa wa mirengo mbalimbali kutangaza bayana kuanzisha mikakati ya kuwashawishi wafuasi wao kujitokeza kujisajili, idadi kubwa ya Wakenya inaonekana kutojihusisha na mchakato huo.

Katika wiki ya pili IEBC ilitangaza watu milioni 1.5 walijisajili kuwa wapiga kura ambayo ni asilimia 25 ya idadi ambayo tume hiyo inapania kusajili katika zoezi zima.

Wiki ya tatu inaripotiwa takriban watu milioni 2.5 wamejisajili kuwa wapiga kura. Sasa ni bayana kuwa watu milioni sita waliotarajiwa kusajiliwa na IEBC katika kipindi cha mwezi mmoja hawatafikiwa.

Lakini huku Tume hiyo inayoongozwa na Wafula Chebukati ikishikilia kuwa ukame na ukosefu wa usalama maeneo mengine ndizo sababu za wakenya wengi kutosajiliwa.

Lakini Wakenya wanaeleza kukatishwa tamaa na jinsi mchakato mzima unavyoendeshwa. Vile vile wanaelezea kukerwa kwao vile wanasiasa walivoupa mchakato mzima kipaumbele na kuacha kushughulikia masuala mengine yanayo waathiri Wakenya.