Hii ni licha ya tume ya kupambana na ufisadi nchini humo kutaka washukiwa wa ufisadi na uhalifu kufungiwa nje ya zoezi hilo kulingana na katiba ya nchi hiyo.
IEBC imesema kwamba haiwezi kuwazuia wagombea hao bila kupata maamuzi ya mahakama kuhusu watuhumiwa.
Taasisi ya kupambana na ufisadi nchini Kenya EACC, iliandika barua kwa tume huru ya uchaguzi IEBC, ikiitaka kutoidhinisha majina ya wagombea zaidi ya 240, wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali zikiwemo za ufisadi.watuhumiwa wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya pesa wakati wakiwa ofisini katika ngazi za juu serikalini.
Wagombea waliotajwa
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni wagombea wa urais, magavana 63, maseneta, wabunge na wawakilishi wa akina mama.
Mgombea wa urais Justus Juma, anadaiwa kuwasilisha stakabadhi za mtu mwingine akidai ni zake kugombea nafasi hiyo. Gavana Mwangi wa Iria anadaiwa kuwazuia maafisa wa tume ya uchaguzi kumchunguza kutokana na kashfa za ufisadi, Aliyekuwa gavana Daniel Waitahala ana kesi ya ufisadi inayoendelea, sawa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero anaandamwa na kesi ya wizi wa mamilioni ya pesa. Gavana wa Garissa Ali Korane, ana kesi ya wizi wa shilingi milioni 233. Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko alipigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na bunge la jimbo la Nairobi kutokana na ufisadi wa mamilioni ya pesa, aliyekuwa katibu mkuu katika wizara ya vijana anashutumiwa kwa wizi wa shilingi milioni 467 za Kenya, sawa na Gavana Ann Waiguru, miongoni mwa wengine.
Wengine waliotajwa ni gavana wa Busia Sospeter Ojamoong ambaye sasa anagombea ubunge, na Gavana wa Machakos Alfred Mutua.
Kulingana na wachambuzi wa siasa, japo hatua ya kuwazuia washukiwa kugombea nafasi hizo inafaa, imekuja kwa wakati mbaya na huenda ikatafsiriwa moja kwa moja kama ya kuandamwa kisiasa, ikitiliwa maanani kwamba kuna madai ya mapendeleo kutoka kwa idara za serikali kuhusu wagombea wakuu wa kisiasa na vyama vya kisiasa, hasa baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza mtu anayempendelea kumrithi. Prof David Monda ni mhadhiri wa siasa katika chuo kikuu cha City, New York
“mpiga kura au wanaharakati wa marengo yote inayohusika katika uchaguzi huo wataona kwamba kuna mkono wa serikali au kuna chenga zinapigwa na mambo hayasimamiwi kwa njia ya wazi. Changamoto kama hizi ndizo zilipelekea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 kutokana na madai kwmaba uchaguzi haukuwa wa kweli na haki.” Amesema Prof David Monda.
Katiba inasemaje kushu washukiwa wa uhalifu na ufisadi katika uchaguzi?
Tume ya maadili inadai kwamba wagombea wengi wamevunja ibara ya 6 ya katiba ya taifa. Lakini wachambuzi wanasema iwapo ibara hiyo itafuatwa inavyostahili, basi hakutakuwa na uchaguzi Kenya, maana wagombea wengi hawatimizi mahitaji ya ibara hiyo.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati, amesisitiza kwamba hatafanya kazi ya mahakama ya kuhukumu washukiwa.
“Ibara ya 6 kweli ipo kwenye katiba lakini wanasiasa wengi sana wana mapungufu na hawakithi masharti ya ibaya hiyo. Wengi sana wana kashfa za ufisadi lakini wanagombea nafasi katikauchaguzi na vyama vyao vinawaunga mkono. Maadhili ya kitaifa ni kama tumeyasahau. Itakuwa vigumu sana kutekeleza ibara hiyo ya sheria” ameendelea kusema Prof Monda.
Jukumu la magavana katika maendeleo ya Kenya
Magavana wana jukumu kubwa la kufanikisha ugatuzi, na wanapokea kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa serikali kuu kufanikisha maendeleo mashinani.
Baadhi ya wagombea vile vile wanadaiwa kukosa kujiuzulu nafasi zao serikali kufikia Februari 9 mwaka huu inavyohitajika kikatiba ndipo waruhusiwe kugombea nafasi mbali mbali.
Katika miaka 10 ya ugatuzi nchini Kenya, kesi kadhaa za wizi wa mabilioni ya pesa za uma, matumizi mabaya ya ofisi, na ufisadi uliokithiri vimeripotiwa. kesi kadhaa zimefunguliwa mahakamani lakini kakuna aliyeadhibiwa, au kulazimishwa kurudisha pesa zilizoibwa.
Kulingana na tume ya kupambana na ufisadi Kenya, shilingi bilioni 608 sawa na asilimia 7.8 ya mapato ya jumla ya nchi, huibwa kila mwaka.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC