Tume yatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu DRC

Rais wa DRC, Joseph Kabila.

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC imetangaza Jumatano kwamba uchaguzi wa urais uliochelewa kufanyika kwa muda mrefu hauwezi kufanyika hadi mwaka 2019.

Tangazo hilo kwa mujibu wa wachambuzi wa kisiasa inakwenda kinyume na mkataba ulioafikiwa na upinzani kwamba uchaguzi utafanyika mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.

Upinzani haraka uliita hatua hiyo ni kunyakua madaraka wakimshutumu Rais wa DRC Joseph Kabila kwa kutaka kujiongezea muda wa utawala wake. Kulikuwepo na ishara kwamba uchaguzi utarudishwa nyuma hadi mwaka 2018 lakini tangazo jipya liliongeza hali ya mvutano ambayo tayari ipo katika taifa hilo la Afrika ya kati.

Muda wa Rais Kabila kuwepo mamlakani ulishaisha tangu mwezi Disemba mwaka 2016 lakini mahakama inaeleza kwamba kiongozi huyo anaweza kuendelea kukaa mamlakani hadi uchaguzi ujao utakapofanyika. Rais wa tume ya uchaguzi Corneille Nangaa alisema Jumatano kwamba ghasia zinazotokea kati kati ya nchi ndio sababu ya kucheleweshwa kwa uchaguzi kwani hawawezi kuwasajili wapiga kura.