Trump aahidi kuvunja mkataba wa biashara wa TPP siku ya kwanza ofisini

Magari yakipita mbele ya Trump Tower mjini New York, Nov. 21, 2016.

Rais-mteule wa Marekani Donald Trump anasema siku yake ya kwanza tu ofisini atachukua hatua ya kutangaza kuwa Marekani inajitoa katika mkataba wa biashara wa Trans-Pacific Partnership, moja ya mfululizo wa hatua zake za "kuiweka Amerika kwanza."

Katika ujumbe wake wa video uliwekwa kwenye mtandao wa Youtube, Trump alisema mkataba huo, maarufu kama TPP, unaweza kuwa "janga" kubwa kwa Marekani.

Donald Trump akizungumza kupitia mtandao wa Youtube

​Muda wote wa kampeni yake Trump alisema kuwa anapinga mkataba huo, ambao unahusisha nchi 12 za Asia-Pacific, pamoja na mkataba wa biashara wa nchi za Amerika kaskazini, Canada na Mexico, unaojulikana kama NAFTA. Alijisifu kuhusu uwezo wake wa kupata makubaliano ambayo yatakuwa na tija zaidi kwa Marekani.

Mawaziri kutoka nchi za TPP walitia saini mwezi Februari mwaka huu, wakisema kuwa lengo lao ni "kuongeza tija ya pamoja, kuongeza nafasi za kazi, na kukuza maendeleo endelevu ya uchumi kwa mataifa yetu yote."

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe akikutana na Rais-mteule Donald Trump, New York, Nov. 17, 2016.

Majibu ya Viongozi wa Nje

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema Jumanne kuwa TPP "haitakuwa na maana bila ya Marekani."

Waziri Mkuu wa New Zealand John Key alisema msimamo wa Trump unasikitisha, lakini kuna njia nyingine mbadala, ikiwa ni pamoja nchi zilizobaki 11 kufikia makubaliano yao wenyewe.

Rais Obama aliunga mkono mkataba huo, lakini Bunge la Marekani halikutoa idhini yake kwa Marekani kujiunga rasmi katika mkataba huo.

Uhamiaji

Ahadi alizotoa Trump Jumatatu kuhusu siku atakapochukua madaraka miezi miwili ijayo haikuwa na mengi kuhusu ahadi alizotoa kwenye kampeni kama vile kujenga ukuta baina ya Marekani na Mexico.

Alisema tu kuwa ataitaka wizara ya kazi kuchunguza "ukiukaji wa visa za kazi ambazo zinaathiri wafanyakazi wa Kimarekani" na kutaka Wizara ya Ulinzi kuja na mpango maalum wa kulinda miundo mbinu ya taifa dhidi ya "mashambulizi ya kimtandao na mashambulizi mengineyo."

Trump amekuwa akikutana na watu kadha mashuhuri Marekani ambao inasemekana wanafikiriwa kuwa katika serikali yake. Miongoni mwa aliokutana nao wiki hii ni pamoja na gavana wa zamani wa Texas Rick Perry, ambaye alikuwa mmoja wa wagombea wa mwanzo katika kinyang'anyiro cha warepublican mwaka jana.

Kellyanne Conway, meneja wa kampeni ya Rais-mteule Donald Trump.

Meneja wa kampeni ya Trump, Kellyann Conway amesema sio kila mtu aliyekutana na Trump katika siku hizi chache atapata kazi katika utawala wake. Lakini, alisema " wote ni watu wanaoaminika sana katika kutoa maoni yao, uzoefu wao na bila shaka mitizamo yao kuhusu hatima ya Marekani."

Trump alitazamiwa kuondoka New York Jumanne au Jumatano kuelekea Florida ambako atasherehekea sikukuu ya Thanksgiving inayofanyika kote nchini Alhamisi.