Trump na washirika wake wanashutumiwa kwa kujaribu kuvuruga matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Georgia ambalo alishindwa na rais Joe Biden.
Anadaiwa kumshurutisha msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, mrepublican, kutafuta kura za kutosha kumpa ushindi ili aendelee kusalia madarakani.
Anashutumiwa pia kuendelea kusema madai ya uongo kwamba uchaguzi mkuu ulikumbwa na udanganyifu na kujaribu kushawishi wabunge wa jimbo la Georgia kutotilia maanani maamuzi ya wapiga kura na kuchagua waidhinishaji feki wa uchaguzi kuidhinisha kwamba Trump alishinda uchaguzi huo kinyume cha sheria.
Mashtaka hayo yanaelezea namna Trump alijaribu kuvuruga mashine za kupiga kura katika jimbo la Georgia.
Wengine walioshitakiwa pamoja na Trump ni pamoja na Mark Meadows, wakili wa Trump Rudy Giuliani, aliyekuwa mwanasheria katika wizara ya sheria wakati wa Trump Jeffrey Clark ambaye alikuwa msitari wa mbele katika kutaka kubatilisha matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Georgia.
Mawakili waliokuwa wakimshauri Trump wakiwemo John Eastman, Sidney Powell na Kenneth Chesebro pia wamepatikana na makosa ya kujibu.
Wote walioshitakiwa wataruhusiwa kujiwasilisha mahakamani adhuhuri Augosti 25.
Waendesha mashtaka wanapanga kuanza kesi hiyo katika muda wa miezi sita kuanzia leo.