Trump na wademocrat bado hawajaafikiana kufungua serikali kuu

Jengo la bunge la Marekani linavyoonekana wakati serikali kuu imefungwa

Mpango wa Democrat wa matumizi haujumuishi fedha zozote kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico kama anavyotaka Rais Trump

Kufungwa kwa baadhi ya idara za serikali kuu ya Marekani kumeingia siku ya 11 ulipoingia mwaka mpya wa 2019 huku wabunge na Rais Donald Trump bado hawajaafikiana juu ya matakwa ya rais ya kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Wademocrat katika baraza la wawakilishi wanasema wakati wanapochukua udhibiti wa bunge siku ya Alhamis wanapanga haraka kuidhinisha mswada wa kufunguliwa tena robo ya operesheni za serikali kuu ambazo zimefungwa tangu Disemba 22 mwaka 2018 japokuwa uidhinishwaji kwenye baraza la seneti una mashaka.

Mpango wa Democrat wa matumizi unajumuisha kutoweka fedha zozote kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kama anavyotaka Rais Trump.

Rais Donald Trump

Trump aliandika kwenye Twitter, "wademocrat kama nilivyobashiri hawajaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta mpya. Hilo lilitarajiwa". Tatizo ni kwamba bila ya ukuta hakutakuwa na usalama wa kweli wa mpakani na nchi yetu lazima hatimaye iwe na mpaka imara na madhubuti.