Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton walishambuliana kwa maneno kila mmoja akimshutumu mwenzie Jumanne kwamba hawezi kuongoza mapambano ya Marekani katika kulitokomeza kundi la wanajihadi wa Islamic State.
Trump ambaye ni bilionea nchini Marekani anayetafuta fursa ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia White House alidai Clinton anatoa taarifa pungufu kuhusu kitisho cha ugaidi, kwa maana hiyo hastahili kuwania urais wa Marekani.
Bwana Trump aliwaambia wanafunzi wa chuo kwenye mkutano wa kisiasa katika jimbo la North Carolina-NC ambalo ni jimbo muhimu kwa wagombea wote wa urais hivi sasa akisema kwamba “pale Clinton anaposema upinzani wangu kwa kundi la ugaidi la Islamic State, anatoa msaada na kumliwaza adui, tunafahamu kwamba Hillary Clinton kwa mara nyingine alijieleza kwamba hastahili kuingia White House”.
Mgombea huyo wa urais kwa chama cha Republican aliendelea kusema kuwa “matamshi yake sio tu hayana msingi lakini hayafikii hadhi ya nafasi anayowania ya kuongoza nchi”.
Wakati huo huo Clinton, aliyewahi kushika nafasi ya waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani na hivi sasa anajaribu kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini Marekani alisema Jumatatu kwamba matamshi ya Trump ya kupinga uislam yamemfanya Trump “mkuu wa kuandikisha” magaidi.
Lakini Trump aliwaambia wafuasi wake katika jimbo la North Carolina kwamba “mimi ninachukua msimamo mkali” itakuaje niwe chombo cha kuandikisha magaidi.”
Clinton amesitisha kampeni Jumanne akijiandaa kwa mdahalo wa kwanza wa urais na mpinzani wake Trump unaotarajiwa kufanyika Jumatatu ya Septemba 26.