Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, mgombea urais wa Demokrat katika uchaguzi wa Novemba, na mpinzani wake wa chama cha Republikan, Rais wa zamani Donald Trump, Alhamisi walikubaliana kushiriki mdahalo wa televisheni hapo Septemba 10 kwenye kituo cha televisheni cha ABC News.
NBC News pia inajadiliana kuhusu uwezekano wa mdahalo wa pili na timu za kampeni zote mbili.
Wakati huo huo, Trump amesema katika mkutano mrefu na wanahabari kwamba kituo cha CBS News kimekubali kuandaa mdahalo wa wagombea wenza , Seneta wa Ohio, JD Vance, wa Rupublikan na mwenzake Gavana wa Minnesota Tim Walz wa Demokrat.
Trump amesema pia amekubali tarehe ya mjadala wa Septemba 4 wa Fox News, ambapo safu ya wachambuzi wa kihafidhina wanapendelea kuchaguliwa kwake, lakini kampeni ya Harris haijakubali.