Trump awataka wabunge kukataa muswada wa ufadhili wa serekali

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, Jumatano amewataka  wabunge wa Marekani kuukataa mswada wa ufadhili wa muda kwa bajeti baada ya Ijumaa, na hivyo kuongeza uwezekano wa kufungwa kwa sehemu ya serekali kuu.

Trump na Makamu wa Rais mteule JD Vance, wametoa wito kwa wabunge kupitisha mswada wa matumizi ya muda tofauti na ule uliopitishwa Jumanne, bila kile walichokiita zawadi za Demokrat.

Trump pia alitoa wito kwa wabunge kutumia mswada huo kushughulikia ukomo wa deni la taifa, akiingiza kipengele kipya chenye utata katika mchakato huo.

Hilo linaweza kuhatarisha juhudi za kuepusha kufungwa kwa serekali ambako kutavuruga kila kitu kuanzia usafiri wa anga hadi masuala ya ulinzi na usalama kabla ya likizo ya Krismasi.

Itakuwa mara ya kwanza kufungwa kwa serikali toka ile iliyoongezwa ya Desemba 2018 mpaka 2019, wakati wa muhula wa kwanza wa miaka minne wa Trump.