Trump ateuwa Thomas Homan kuwa mkuu wa uhamiaji

  • VOA News

Thomas Homan ambaye ameteuliwa na Trump kuwa mkuu wa uhamiaji kwenye serikali yake mpya.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Thomas Homan, ambaye alikuwa kaimu mkuu wa uhamiaji kwenye muhula wake wa kwanza, kama mkuu wa uhamiaji kwenye serikali yake mpya.

Tanagazo hilo linaonekana kama hatua ya kutimiza ahadi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu. Kupitia mtandao wake wa Truth Social Jumapili, Trump alisema kuwa Homan mwenye umri wa miaka 62 atasimamia mipaka ya nchi kuanzia mpaka wa Mexico upande wa kusini hadi kaskazini karibu na Canada.

Aliongeza kusema kuwa hana shaka kwamba Homan atafanya kazi nzuri, na kwamba amemfahamu kwa muda mrefu, akiamini kuwa “anafaa zaidi kulinda mipaka yetu.” Chombo kimoja cha habari cha Marekani kimeripoti kwamba Trump pia anatarajiwa kuteuwa Stephen Miller, mwenye msimamo mkali wa uhamiaji kama naibu mkuu wa utawala kwa ajili ya sera.

Makamu mteule wa Trump JD Vance amesifu uwezekano wa Miller mwenye umri wa miaka 39 kujiunga kwenye utawala wa Trump. Trump pia ameteua mmoja wa wanaharakati sugu wa Repablikan kwenye Bunge, mwakilishi Elsie Stefanik wa New York kuwa balozi mpya wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.

Stefanik mwenye umri wa miaka 40 alichaguliwa kwenye baraza la wawakilishi 2015, wakati huo akiwa mwenye msimamo wa kisiasa wa wastani, lakini baadaye akawa mtetezi mkubwa wa Trump.