Trump akata rufaa kutetea amri ya katazo la kusafiri

Rais Trump

Uongozi wa Trump umekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya serikali kuu ambayo imezuia rekebisho la amri ya kupiga marufuku kwa nchi sita zenye Waislamu wengi.

Wizara ya Sheria ya Marekani imesema katika kufungua kesi Ijumaa inakata rufaa dhidi ya uamuzi wa jaji wa mahakama ya wilaya ya Marekani, Theodore Chuang katika jimbo la Maryland.

Uamuzi huu unatokea siku mbili baada ya mahakama ya serikali kuu Maryland pamoja na mahakama nyingine Hawaii kuzuia baadhi ya katazo la kusafiri la Trump, na mahakama zote mbili kuamua amri hiyo inawabagua Waislamu.

Chuang alitoa katazo la dharura kusimamisha sehemu ya amri ya kiutendaji ya Trump iliyokuwa imezuia kwa muda wasafiri kutoka nchi sita zenye Waislamu wengi kuingia Marekani. Jaji huyo hakuigusa sehemu ya pili ya amri hiyo iliyokuwa inakataza kwa muda wakimbizi kuja Marekani.

Jaji mwengine Hawaii ameondoa sehemu zote za katazo hilo la Trump la kusafiri.

Kesi hiyo sasa inakwenda kwenye mahakama ya rufaa huko Richmond, Virginia