Rais mteule Donald Trump, Jumapili amesema anapanga kutoa amri ya kiutendaji ambayo itaipatia kampuni mama ya mtandao wa TikTok, yenye makao yake China muda zaidi wa kutafuta mnunuzi aliyeidhinishwa kabla ya mtandao huo maarufu wa video kukabiliwa na marufuku ya kudumu ya Marekani.
Trump alitangaza uamuzi huo katika ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii Truth, huku mamilioni ya watumiaji wa TikTok nchini Marekani wakiamka na kugundua kuwa hawawezi tena kutumia mtandao huo wa TikTok.
Kampuni za Google na Apple ziliondoa programu ya TikTok, kwenye maduka yao ya kidijitali ili kutii sheria ya serikali iliyowataka kufanya hivyo endapo kampuni mama ya TikTok ByteDance haikuuza operesheni zake Marekani kwa mnunuzi aliyeidhinishwa mpaka kufikia Jumapili.
Amesema amri yake ya kiutendaji itaongeza muda kabla ya marufuku ya sheria kuanza kutekelezwa na kuthibitisha kwamba hakutakuwa na matokeo yoyote kwa kampuni ambayo imesaidia kuzuia TikTok kutumika kabla ya agizo lake.