Trump atakiwa kukemea ubaguzi dhidi ya Waislamu

Rais Donald Trump

Rais Donald Trump Jumanne amelaani hadharani vitendo na kauli za chuki dhidi ya Wayahudi, baada ya kuwepo wimbi la vitisho vya mabomu dhidi ya vituo vya jamii ya Wayahudi.

Lakini Waislamu wengi Marekani wameudhika kwamba rais hajachukua hatua alizochukua kulaani chuki dhidi ya Wayahudi, kushughulikia malalamiko juu ya chuki dhidi ya Waislamu.

Rais Donald Trump amekosolewa kwa kutotumia fursa mara nyingi kulaani kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi.

Mwandishi wa VOA ameripoti kuwa rais amekuwa mwazi Jumanne aliposema: “ Vitisho dhidi ya jamii zetu za kiyahudi na vituo vyao ni jambo linalotisha na lenye kuumiza mioyo.”

Mwandishi ameelezea kuwa Waislamu wengi wa Marekani hivi sasa wanatarajia kuwa rais atachukua hatua, sawa na alizochukuwa kulaani chuki dhidi ya Wayahudi, kukabili tatizo linaloongezeka la matukio ya kuwachukia Waislamu nchi nzima. Lakini wamesema bado hawana matumaini.

Corey Saylor wa Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu amesema: “ Rais kwa jumla amekuwa kimya baada ya uchaguzi, kumekuwa na wimbi la jinai za chuki dhidi ya dini, mila, makabila madogo, na ukoo, hilo linatosha kuwaonyesha watu kwamba hatua zaidi zinatakiwa zichukuliwe.”

Makamu wa Rais Mike Pence

Saylor amesema lazima maneno yafatiwe na vitendo kama vile mfano aliyo onyesha Makamu wa Rais, Mike Pence, akisaidia katika juhudi za kusafisha makaburi ya Wayahudi baada ya kuharibiwa na watu wenye chuki dhidi yao huko St. Louis, Missouri:

Hakuna nafasi ya kueneza chuki hapa Marekani, au vitendo vya ubaguzi vinavyohusisha kuvunja amani au chuki dhidi ya Wayahudi.”

Mwandishi amesema sababu ya watu kukata tamaa hasa Waislamu, inatokana na kauli za Trump na baadhi ya washauri wake ambayo inaonyesha vita dhidi ya ugaidi katika msamiati wa kidini, inajumuisha pendekezo la Trump wakati wa kampeni linalokataza Waislamu kuingia nchini.

“Donald Trump ametaka kuzuiwa kabisa waislamu wanaoingia Marekani mpaka pale wawakilishi wetu watapofahamu kitu gani kinachoendelea.” Japokuwa Trump aliacha kutumia kauli hiyo, bado ipo katika tovuti yake imesema repoti yake.

Hata hivyo maafisa wa White House wamekataa kwamba kauli hizo za Trump hazionyeshi chuki na Waislamu. Msemaji Michael Short ameiambia VOA “ Kutambua hatari ya ugaidi wa kiislamu hakuwezi kumfanya mtu kuwa anawachukia Waislamu.”