Trump atishia kufunga serikali kuu

Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump alitishia Jumapili kufunga serikali kuu kama bunge halitapitisha mswada wa fedha za ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico ili kuwazuia wahamiaji haramu.

Trump amedai Democrat wanahitajika kumpigia kura hiyo ya usalama wa mpaka inayojumuisha ujenzi wa ukuta na mabadiliko ya sera za uhamiaji

Kiongozi huyo wa Marekani amesema upinzani wa chama cha Democrat unahitajika kumpigia kura hiyo kwa ajili ya usalama wa mpaka kura ambayo inajumuisha ujenzi wa ukuta na mabadiliko mengine magumu ya sera za uhamiaji.

Lakini hatua hiyo ilikwamishwa na mgawanyiko wa kundi la wabunge walio wengi wa-Republican, pamoja na wa-Democrat walioungana pamoja ikiwa ni mara mbili katika wiki za karibuni ambapo wabunge walikataa mabadiliko ya uhamiaji yaliyopendekezwa na Rais Trump.

Trump aliapa kujenga ukuta wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2016, akisema huwenda ukagharimu zaidi ya dola bilioni 20, lakini bunge limechangia dola bilioni 1.5 pekee kwa ajili ya usalama wa ziada kwenye mpaka.