Rais wa Marekani Donald Trump alisema Jumamosi kwamba hajapewa maelezo kuhusu ripoti ya idara ya ujasusi ya serikali kuu ya Marekani-CIA ambayo inahitimisha kwamba mwana mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman aliagiza kuuwawa kwa mwandishi raia wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi lakini atapewa taarifa kamili baadae Jumamosi.
Rais Trump aliwaambia waandishi wa habari huko White House kabla hajasafiri kuelekea jimbo la California “tutazungumza na CIA baadae na masuala mengi menginey. Pia nitazungumza na waziri wa mambo ya nje, Mike Pompeo”. Tathmini ya CIA iliripotiwa kwanza na gazeti la The Washington Post siku ya Ijumaa inapingana na Saudi Arabia ambapo mwendesha mashtaka wa cheo cha juu siku moja kabla alisema mwana mfalme hakuhusika katika mauaji ya jamal Khashoggi.
Maafisa wa Marekani walisema CIA ilihitimisha kwamba maafisa 15 wa Saudi Arabia katika serikali ya Saudi Arabia walipanda ndege kwenda Istanbul na walimuuwa Kashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Uturuki. Kashoggi alikuwa mwandishi wa The Washington Post alimkosoa mwana mfalme kwenye makala zake na aliuwawa kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mwezi Oktoba wakati akijaribu kupata hati rasmi kwa ajili ya ndoa na mchumba wake raia wa Uturuki.