Trump afafanua umuhimu wa waalimu kubeba silaha

Bunduki aina ya AR-15

Rais Donald Trump wa Marekani amefafanua wazo lake la kuwaruhusu waalimu kubeba silaha madarasani ili kuzuia mashambulizi mashuleni.

Amesema anataka kuangalia uwezekano wa “ubebaji silaha kwa kificho kwa walimu wenye maarifa ya kutumia silaha kwa wale wenye kupitia jeshini au wenye mafunzo maalum.

Hilo limekuja siku moja baada ya kuwepo hali ya masikitiko wakati wa mazungumzo ya Trump na wanafunzi walioguswa na matukio hayo ya mauaji mashuleni pamoja na wazazi wao.

Trump katika ujumbe wake wa tweets amesema “ ni asilimia 20 tu ya waalimu bora, ni wengi, sasa wataweza kujibu mashambulizi ya silaha iwapo mtu mkatili ambaye hayuko timamu atapokuja shuleni kwa nia ya kuwadhuru wengine.”
Rais Trump alisema hayo wakati alipokuwa katika mjadala maalumu huko White House uliokuwa na hamasa nyingi ambapo wanafunzi na wazazi walioguswa na mashambulizi hayo ya bunduki nchini Marekani walihudhuria.

Rais alisema huenda pia wakaweka wanajeshi wa zamani katika shule zote jambo ambalo linaweza kutatua matatizo ya mashambulizi ya bunduki shuleni.

Rais wa Marekani, Donald Trump

Wakati mjadala wa bunduki ukiendelea nchini Marekani, Rais Trump pia anafikiria kuwepo na udhibiti wa umri wa ununuzi wa silaha kutoka miaka 18 hadi 21 ikiwemo silaha aina ya AR-15 iliyotumika kwenye shambulizi katika shule ya Florida jambo ambalo chama cha wamiliki wa silaha Marekani-NRA wanalipinga vikali.

Sauti ya Amerika-VOA ilizungumza na mchambuzi wa masuala ya siasa Profesa Charles Bwenge wa chuo kikuu cha Florida, Marekani na kumuuliza hatua ya NRA inatoa picha gani wakati huu kwa utawala wa Rais Trump na wa-Marekani kwa jumla.

Your browser doesn’t support HTML5

Mahojiano ya VOA na Profesa Charles Bwenge wa Florida, Marekani

Mjadala mkali juu ya umiliki wa silaha Marekani umeibuka upya kufuatia shambulizi la bunduki lililofanywa na Nikolas Cruz wiki iliopita katika shule ya sekondari ya Marjory Stoneman Douglas na kuuwa watu 17 katika jimbo la Florida.