Trump akataa kujibu masuali ya mwendesha mashtaka katika uchunguzi kuhusu biashara yake

Rais wa zamani Donald Trump akielekea kwa ofisi ya mwendesha mashtaka mjini New York, Agosti 10, 2022. Picha ya Reuters

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump Jumatano amekataa kujibu masuali katika uchunguzi kuhusu utaratibu wa biashara ya familia yake, akitumia haki yake ya kikatiba.

Trump alichukua msimamo mkali dhidi ya uchunguzi unaoendeshwa na mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la New York, Laetitia James, ambaye anataka kujua ikiwa Trump alipandisha thamani ya hoteli zake, viwanja vya gofu na nyumba zake za kukodiwa ili apate mikopo ya riba nafuu, huku akipunguza thamani ili kupata punguzo la kodi.

“Nilikataa kujibu masuali chini ya haki na fursa zinazotolewa kwa kila raia chini ya katiba ya Marekani, Trump amesema katika taarifa ambapo alimshtumu James kuwa “mwendesha mashtaka aliyeasi na asiyedhibitiwa”, ambaye anaendelea kufanya ulipizaji kisasi dhidi yake.

James alisema uchunguzi wake uligundua ushahidi muhimu kwamba shirika la Trump, linalosimamiwa na rais huyo wa zamani, lilitumia ulaghai kuhusu thamani ya mali zake.