Trump ajibizana na Jaji Mkuu Roberts

Rais Trump na jaji Roberts

Jaji mkuu wa Marekani John Roberts amepuzilia mbali shutuma za Rais Trump dhidi ya jaji aliyeamuru baadhi ya wahamiaji wasifurushwe kutoka Marekani. Trump alimtaja jaji huyo kama "jaji wa Obama."

Katika taarifa yake iliyotolewa na mahakama ya juu kwa vyombo vya habari vya Marekani Jumatano, Jaji mkuu Roberts alisema hakuna majaji wa Obama, hakuna ma jaji wa Bush au wa Clinton, akizungumzaia marais watangulizi wa Trump.

“Tunao majaji wazuri sana ambao wanafanya kazi kwa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayefika mbele yao mahakamani, anatendewa haki,” alieleza Jaji Roberts.

Rais trump hakuchelewa kumjibu jaji huyo mkuu. Aliandika kwenye twitter: “samahani Jaji Mkuu John Roberts, hakika wapo majaji wa Obama, na mara nyingi maamuzi wanayoyachukuwa ni tofauti ya raia wenye jukumu la kuzingatia usalama wa nchi yetu.”

Taarifa hiyo ya Jaji Roberts imewashangaza wengi wakisema si jambo la kawaida kwa jaji mkuu kutoa jibu la moja kwa moja kwa rais.

Jaji Roberts ndiye alimuapisha Trump alipochukua rasmi hatamu za uongozi mwaka jana.