Rais wa Marekani Donald Trump alisema Alhamisi kwamba hatatumia amri ya kiutendaji kuongeza swali la uraia lenye utata kwenye fomu za sensa katika zoezi la kuhesabu watu litakalofanyika mwaka ujao na ambalo hufanyika kila baada ya miaka 10.
Badala yake Trump atatumia amri hiyo kulazimisha idara za serikali kutoa taarifa kwa wizara ya biashara kuhusu rekodi inazohitaji kutadhmini idadi ya raia na wasio raia hapa Marekani.
Wiki mbili zilizopita, mahakama ya juu ilipinga hatua ya Trump ya kuongeza swali la uraia kwenye fomu ya sensa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 70.
Hata hivyo uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Harvard Harris mwishoni mwa mwezi Juni zilionyesha kuwa hata kama mahakama ingepinga ombi la Trump, angali ana uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa miongoni mwa Wamarekani.
Takwimu zilizochukuliwa awali miongoni mwa wapiga kura zinaonyesha kuwa katika kila Wamarekani watatu, wawili wanaunga mkono hatua ya kuuliza mtu kuhusu uraia wake.