Trump aashiria kukubali kushindwa lakini asema hatakiri kwamba ameshindwa

Donald Trump - Rais wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ameonekana kukubali kwamba alishindwa katika uchaguzi mkuu lakini akawa mwepesi wa kusema kwamba hatakubali kushindwa.

Trump ameandika hayo kwenye twitter, wakati rais mteule Joe Biden akiwa anaendelea na mikakati yake ya kukabiliana na janga la virusi vya Corona, akitarajiwa kukutana na wakurugenzi wa kampuni zinayotengeneza chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Hayo yanajiri wakati zoezi la kurudia kuhesabu kura katika jimbo la Georgia likionyesha kwamba hakuna udanganyifu uliofanyika katika uchaguzi wa jimbo hilo ambalo Joe Biden ametabiriwa kushinda.

Shinkizo linaendelea kutolewa kwa rais Donald Trump kukubali kushindwa na kuruhusu mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa Joe Biden kufanyika kwa ajili ya usalama wa nchi na kufanikisha juhudi za kukabiliana na janga la Corona.