Trump aahidi kuzungumza na Putin hivi karibuni kuhusu vita vya Ukraine

  • VOA News

Picha za maktaba za Rais wa Marekani Donald Trump (Kushoto), na mwenzake wa Russia Vladimir Putin.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Alhamisi kwamba hivi karibuni atazungumza na mwezake wa Russia Vladimir Putin ili kujaribu kumshinikiza amalize vita vilivyodumu kwa karibu miaka mitatu na jirani yake Ukraine.

“Mamilioni ya vijana wamepoteza maisha. Hilo halifai,” Trump wakati akiongea kwa njia ya video kutoka Washington aliambia viongozi wa kimataifa wa biashara wanaohudhuria Kongamano la Kimataifa la Biashara mjini Davos, Uswizi. Alisema kuwa “Ukraine ipo tayari kwa makubaliano,” ingawa hakuna mazungumzo ya amani yaliyotangazwa. “Vita hivyo visingelianzishwa.” Alisema.

Trump ambaye amekuwa ofisi kwa siku 3 za muhula wake wa pili huko White House alisema kwamba atauliza Saudi Arabia pamoja na shirika la Mataifa yanayouza Mafuta OPEC, wapunguze bei za mafuta za kimataifa ambazo sasa zipo kwenye dola 77 kwa pipa, ili kudumaza mapato ya Russia ya mafuta, yanayotumika kufadhili vita vya Ukraine. “Iwapo bei za mafuta zitashuka, vita vya Ukraine vitamalizika mara moja,” alisema Trump. “Ni muhimu kwa hilo kufanyika, na huu ndio wakati,” aliongeza kusema.

Matamshi hayo mapya ya Trump yamekuja siku moja baada ya kuelezea mzozo huo kuwa ‘vita vya kusikitisha,’ na kuambia Putin kupitia ujumbe wa mitandao ya kijamii kwamba iwapo hatavimaliza, basi Marekani itaweka ushuru mpya pamoja na vikwazo kwa bidhaa za Russia kuelekea mataifa ya Magharibi.