Tinubu aapishwa kuwa rais wa Nigeria

Bola Tinubu, Jumatatu amekuwa rais wa Nigeria katika kipindi cha changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa nchini humo ambayo ina watu wengi zaidi barani Afrika.

Hali hiyo inawaacha baadhi ya wananchi wakiwa na matumaini ya maisha bora na wengine kuwa na mashaka kuwa serikali yake itafanya vyema zaidi kuliko ile mtangulizi wake.

Maelfu ya Wanigeria na wakuu kadhaa wa serikali walihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Tinubu mwenye umri wa miaka 71 katika mji mkuu wa Abuja.

Anamrithi Rais Muhammadu Buhari kuongoza nchi ambayo ifikapo mwaka 2050 inatabiriwa litakuwa taifa la tatu kwa idadi ya watu duniani, likifungamana na Marekani baada ya India na China.

Tinubu, gavana wa zamani wa Lagos, ambayo ni kitovu cha uchumi wa Nigeria, ameahidi kuendeleza juhudi za Buhari za kidemokrasia kwa raia katika nchi ambayo inakabiliwa na changamoto za kiusalama, umaskini uliokithiri na njaa.