Michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika msimu wa 2 wa mtoano ilianza kwenye Uwanja wa Kigali Arena siku ya Jumamosi.
Katika mchezo wa ufunguzi, Petro de Luanda ya Angola iliwashinda AS Salé ya Morocco kwa jumla ya pointi 102-89. Katika robo fainali ya pili, FAP ya Cameroon iliwashinda timu wenyeji REG ya Rwanda kwa pointi 66-63.
Timu ya REG ya Rwanda ilikuwa nyuma lakini ilirudi mchezoni na katika dakika za mwisho karibu waende muda wa ziada lakini jaribio la Thomas Jr. la kufunga pointi tatu lilikwama Na Cameroon wakaibuka kidedea kwa kuwatoa timu wenyeji kwa pointi 66-63.
Na katika michezo ya Jumapili, mabingwa wa Tunisia US Monastir walimenyana na Cape Town Tigers ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza ambapo Tunisia walitawala mchezo huo na kushinda kwa jumla ya pointi 107-67.
Na baadaye siku hiyo, mabingwa watetezi wa BAL Zalamek ya Misri waliwafungashia virago Seydou Legacy Athletique Club (SLAC) ya Guinea kwa jumla ya point 66-49.
Michezo ya mwishoni mwa juma hili imeingiza timu nne katika nusu fainali. Petro de Luanda, FAP, US Monastir na Zalamek na timu hizo zitamenyana katika nusu-fainali, itakayofanyika Uwanja wa Kigali Arena Mei 25.