Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema Alhamisi kuwa kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Syria ni kitendo cha uchokozi na ukiukaji wa uhuru.
Maono hayo yamekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson kuelezea mipango yake katika hotuba aliyoitoa Jumatano akifafanua kwanini Marekani itaendelea kujihusisha kidiplomasia na kijeshi nchini Syria hata baada ya kulishinda kundi lenye msimamo mkali la Islamic State.
Marekani imeongoza ushirika wa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya malengo ya Islamic State nchini Syria na Iraq tangu mwaka 2014, na Pentagon imesema mwezi Desemba kuna takriban wanajeshi 2,000 wa Marekani nchini Syria.
Tillerson alijadili njia za kusonga mbele kwa Marekani nchini Syria katika tukio kituo kinachoelemea upande wa waconservative kwenye Hoover Institute. Aliorodhesha sababu kadhaa kwanini ni muhimu kwa Marekani kubakia katika nchi iliyogubikwa na vurugu, ikiwemo kuzuia kuibuka tena kwa makundi ya kigaidi ya Islamic State na Al-Qaida.
“Hatuwezi kuruhusu historia ijirudie yenyewe nchini Syria,” amesema Tillerson, akizungumzia kile alichokitaja kama makosa yaliyofanywa na utawala wa Obama katika kuondoa wanajeshi wa Marekani mapema mno nchini Iraq na kushindwa kuleta uthabiti nchini Libya baada ya mashambulizi ya anga ya NATO ambayo yamepelekea kuondolewa mamlakani kwa marehemu rais Moammar Gadhafi.
Tillerson amesema kuna sababu nyingine pia kwa Marekani kubaki na kuendelea kujihusisha nchini Syria.
“Kuwaondoa wanajeshi wote wa Marekani nchini Syria kwa wakati huu kutamsaidia Assad. Uthabiti, umoja na uhuru wa Syria hatimaye vitapatikana baada ya uongozi wa Assad ili kupatikana mafanikio. Kuendelea kuwepo kwa marekani kutahakikisha kuishinda ISIS kabisa na pia kufungua njia kwa mamlaka halali za kieneo ili kuendelea utawala wa majimbo kwa maeneo ambayo yatakombolewa,” amesema Tillerson.