Mahakama ya Sweden, Jumatano ilimpiga faini mwanaharakati wa masuala ya mabadiliko ya hewa Greta Thunberg, kwa mara nyingine tena kwa kutotii polisi wakati wa maandamano ya mazingira ya Julai kusini mwa nchi.
Mahakama ya wilaya ya Malmo ilimuamuru kulipa faini ya krone 2,250 sawa na dola 206 za Marekani.
Thunberg, ambaye tayari alikuwa amepigwa faini kwa kosa kama hilo, alishiriki katika maandamano ya mazingira ya Julai 24 kwenye kituo cha mafuta cha Malmo, ambapo wanaharakati walizuia kwa muda njia ya kituo hicho kwa kukaa chini na kuondolewa na polisi.
Septemba 15, alishtakiwa kwa kutotii vyombo vya sheria kwa kukataa kutii polisi wakimtaka aondoke eneo la tukio.
Aliburutwa na maafisa wawili waliovalia sare.
Thunberg, 20, amekiri ukweli wa mambo lakini alipinga kuwa na hatia, akisema mapambano dhidi ya sekta ya mafuta yalikuwa ya kujilinda kutokana na tishio lililopo na la dunia la mabadiliko ya hali ya hewa.