Theluji kubwa isiyo ya kawaida ilisababisha usumbufu mkubwa katika barabara za Afrika Kusini leo Jumamosi huku watu wakiwa wamekwama nyakati za mchana baada ya kukaa usiku kucha kwenye magari yao.
Barabara kuu ya N3 inayounganisha Johannesburg na mji wa pwani wa mashariki wa Durban ilikuwa moja ya barabara zilizoathiriwa vibaya sana na sehemu kadhaa zilifungwa, na hata njia za mbadala hazipitiki, maafisa walisema.
Huduma za dharura zilikuwa zikifanya kazi ya kuwafikia watu katika magari yao lakini bado haijabainika ni wangapi walioathirika na walikuwa katika hali gani, meneja wa shughuli za kulipia ushuru katika bara bara ya N3 Thania Dhoogra aliliambia shirika la utangazaji la ENCA.