Tetemeko La ardhi la sababisha vifo na majengo kuporomoka Mexico

Watu wakitoa msaada kwa waathirika wa tetemeko hilo katika jengo lililoanguka Mexico City

Tetemeko kubwa la ardhi la ukubwa wa kipimo cha 'ritcher scale'  7.1 limeikumba Mexico City siku ya Jumanne  na kuangusha majengo pamoja na kuuwa watu kadhaa  na wengine kadhaa wasiojulikana wamekwama katika kifusi.

Saa kadhaa baada ya tetemeko kutokea kwenye eneo la mji mkuu saa za mchana ripoti kutoka serikali kuu ya Mexico na maafisa wa eneo zimeashiria kuwa idadi ya vifo huenda ikavuka 100.

Vifo hivyo vimeripotiwa kutokea eneo kubwa la Mexico City na majimbo jirani ya Morelos, Puebla na Mexico. Kiini cha tetemeko kilikuwa jimbo la Puebla kilomita 123 kusini-mashariki mwa Mexico City.

Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto.

Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto amesema angalau majengo 27 yalianguka katika mji mkuu. Vyombo vya habari katika eneo viliripoti uharibifu mkubwa ikiwemo kukatika kwa umeme na moto katika mji mzima, moja ya eneo la mjini lenye watu wengi duniani.

Raia pamoja na timu za uokozi walikwenda kufanya kazi wakiwatafuta walionusurika. Televisheni za ndani zinaonesha picha za watu wakitumia kila aina ya kifaa kuanzia mashine nzito hadi mikono yao wakifukua vifusi.