Tetemeko la ardhi limetokea magharibi mwa Afghanistan Jumatatu, na kuuwa takribani watu 22, na kujeruhi wengine kadhaa.
Kitovu cha tetemeko hilo lililokuwa na nguvu ya 5.3 kwenye rikta, kilikuwa takriban kilometa 40 mashariki mwa Qala-e-Naw, mji mkuu wa jimbo la Badghis kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha mambo ya jiolojia cha Marekani.
Shirika la habari la Afghanistan la Bakhtar limenukuu mamlaka nchini humo ikisema kwamba wanawake na Watoto ni miongoni mwa walioathirika zaidi. Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.
Vifo vingi na uharibifu mkubwa umetokea katika wilaya ya Qadis ambapo mapaa ya nyumba nyingi za wakazi yameezuliwa. Afghanistan inayokabiliwa na umasikini mkubwa imekuwa ikikumbwa na matetemeko ya ardhi, hasa katika maeneo ya milima ya Hindu Kush inayopatikana karibu na mabonde ya Eurasia na India.