Trump atathmini majina 11 kwa nafasi ya FBI

Rais Donald Trump

Rais Donald Trump tayari anaorodha ya watu 11 anaowafikiria katika nafasi ilioachwa wazi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (FBI) James Comey aliyemfukuza kazi.

Ikulu ya White House imesema hayo Ijumaa na tayari Idara ya Sheria imejiandaa kuanza usaili wa watu hao Ijumaa au siku za wikiendi.

Msemaji wa White House Sean Spicer ametoa muhtasari kwamba Trump atachagua mtu kujaza nafasi mara moja wakati atapompata mtu anayekidhi sifa ambazo anafikiria ni muhimu katika kuongoza FBI.

Hata hivyo uteuzi huo utakuwa na uchunguzi wa kina kwa kuwa Comey alifukuzwa wakati akiongoza FBI kuchunguza iwapo kulikuwako na ushirikiano kati ya kampeni ya urais ya Trump na Russia mwaka 2016.

Wafuatao ni watu 11 ambao wanafikiriwa katika nafasi hiyo:

Ray Kelly

Kelly alikuwa Kamishna wa Polisi wa Jiji la New York kwa muda mrefu kuliko mtu mwengine yoyote.

Mike Rogers

Alikuwa mfanyakazi wa FBI ambaye ameshikilia pia nafasi ya Kiti cha Ubunge cha Michigan mpaka 2015 na pia amewahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Bunge.

Alice Fisher

Fisher alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa kitengo cha Jinai cha Idara ya Sheria chini ya utawala wa Rais George W. Bush.

Trey Gowdy

Gowdy ni Mbunge kutoka South Carolina na pia aliwahi kuwa mwendesha mashtaka wa serikali kuu.

John Cornyn

Ni seneta wa Republikan kutoka Texas na ni mwenye nafasi ya pili katika wadhifa wake kwenye Baraza la Seneti. Kabla ya hapo alikuwa mwanasheria mkuu wa Texas.

Paul Abbate

Abbate amefanya kazi miaka mingi na FBI na hivi sasa anatumikia nafasi ya mkurugenzi mtendaji msaidizi wa Kitengo cha Jinai, Mitandao, Majibu na huduma.

Michael Garcia

Alikuwa ni mwendesha mashtaka huko New York na hivi sasa anatumikia nafasi ya jaji msaidizi katika mahakama ya rufaa ya New York.

John Suthers

Suthers ni mwanasheria mkuu wa zamani wa Colorado na sasa ni meya wa Colorado Springs, Colorado.

Michael Luttig

Luttig, Wakili wa zamani wa Idara ya Sheria na jaji ya mahakama ya rufaa.

Larry Thompson

Thompson alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa Marekani kati ya mwaka 2001 hadi 2003 wakati wa utawala wa Bush.

Andrew McCabe

McCabe amekaimu ukurugenzi wa FBI katika kipindi cha wiki hii baada ya Trump kumfukuza kazi Comey. Ni naibu mkurugenzi wa FBI.