Kuanzia leo Julai 24 tutakuwa tunakuletea makala maalum zinazohusu uchaguzi nchini Kenya na habari mbali mbali zinazohusiana na kampeni zinazoendelea nchini humo. Leo tunamulika kuhusu uchaguzi huo na baadhi ya mambo muhimu ambayo yanayohusu safari kuelekea upigaji kura wa Agosti nane.
Uchaguzi wa mwaka huu ni wa tano tangu kumalizika kwa mfumo wa siasa za chama kimoja Kenya, mwaka 1991. Macho ya wakenya ndani na nje ya nchi yako katika upigaji kura wa Agosti nane ambapo kama inavyoshuhudiwa ushindani ni mkali na kila mgombea amejizatiti kuhakikisha anafanya kampeni kabambe ambazo zitawavuta wapiga kura wengi wampigie yeye.
Ni uchaguzi ambao tutashuhudia wagombea wawili wakuu ambao ni wapinzani wakubwa wakiwania wadhifa wa juu nchini humo. Rais aliyepo mamlakani, Uhuru Kenyatta ambaye anawania kuchaguliwa tena kuiongoza Kenya na aliyewahi kushika wadhifa wa waziri mkuu nchini humo, Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa mkongwe katika historia ya siasa za Kenya.
Ni dhahiri kuwa wagombea hawa wawili wanaowania urais ni wapinzani na washindani wakubwa wa kisiasa katika uchaguzi huu ambao unaelezewa kuwa kila upande umepania kutangaza ilani ya chama chake kwa lengo la kuvutia wapiga kura wengi zaidi ili kuwapa fursa ya kuiongoza Kenya.
Jaji wa mahakama kuu nchini Kenya, Dunstan Omari anasema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na tofauti kubwa hasa katika kumfahamu mpiga kura wa kweli na yule ambaye si wa kweli. Hayo ni miongoni mwa maboresho machache yaliyofanywa katika kuwa na uchaguzi huru, wa haki na wenye hadhi.
Ni dhahiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu una ushindani mkali kati ya vyama viwili vikuu vya siasa licha ya kwamba kuna vyama vingine vidogo na wagombea huru, hali hii inabainisha kuwa mambo yalivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2013 ni tofauti na mwaka huu.
Mbali ya wagombea kuwania nafasi za juu ya uongozi kama vile urais, pia kuna wale ambao wamejikita katika kuwania uwakilishi wa majimbo na kaunti na pia katika nafasi ambazo zimetengwa mahsusi kwa ajili ya wanawake na pia kwa wale ambao wataingia katika baraza la senate.
Lakini yote haya yanafanyika changamoto zikiwa nyingi kuanzia kuwaelimisha wananchi hasa wapiga kura juu yote yaliyo muhimu kuyakumbuka katika siku ya uchaguzi ili kuhakikisha upigaji kura unakuwa wa amani na utulivu hadi yale yanayohusu ni mambo yapi yanaweza kumnyima mpiga kura fursa ya kutumia haki yake ya kikatiba.
Vyombo vya habari, asasi za kiraia na hata mitandao ya kijamii imekuwa mstari wa mbele katika kumuelimisha mpiga kura umuhimu wa kuitumia vyema nafasi yake ya kikatiba. Lakini kuna harakati ambazo zimeanzishwa na kina mama wa Kenya waishio nje ya taifa hilo ambao wameunda muungano maarufu kama Kwitu Breaking Barriers wakiwa na jukumu zito la kuelimisha na kuwasihi wakenya huu ni wakati muafaka wa kuweka uzalendo wa nchi na kuhakikisha amani inadumishwa wakati wa kampeni, upigaji kura na hata baada ya uchaguzi.
Mwakilishi wa Kwitu, Mariam Jarady maarufu kama Mamchi ambaye anaishi Marekani ameelezea jinsi Kwitu ilivyosimama kidete katika kuwasilisha ujumbe wa umuhimu wa amani na utulivu wakati wa uchaguzi na hata baada ya matokeo kupatikana.
Licha ya kwamba kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu tumeona changamoto za kisiasa zikiwasilishwa mahakamani dhidi ya tume ya taifa ya uchaguzi na mipaka – IEBC kuwa haikutumia taratibu zinazostahili katika kuipatia zabuni kampuni moja ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Al Ghurair kuchapisha karatasi za kura, hata hivyo hali ya hewa ya kisiasa imekuwa ni shwari katika kampeni za kisiasa mbali ya kila chama kunadi sera zake ili kuvutia wapiga kura ili kiibuke na ushindi baada ya Agosti nane.
Na utaratibu wa upigaji kura katika uchaguzi huu unaelezewa kuwa umeboreshwa zaidi ili kujaribu kuondoa hitilafu ambazo zimekuwa zikijitokeza jambo ambalo linawatia moyo baadhi ya wapiga kura nchini humo. Mfanyabiashara wa Mombasa, Lillian Njoki ambaye anakumbuka ghasia za baada ya uchaguzi wa 2008. Lakini ana imani kubwa mambo siku ya uchaguzi yatakuwa ya kutia moyo zaidi.
Your browser doesn’t support HTML5