Tanzia ya muigizaji Maureen ‘SASHA’ Wanza

Maureen (Sasha ) akiwa na Kenneth Ambani (Benjamin)

Kifo cha Maureen Wanza kilitokea September 19 2017 akijifungua katika zahanati moja katika Kaunti ya Kilifi Kenya.

Aidha madaktari waliokuwa wanamhudumia wamesema kuwa pia msanii huyo alimpoteza mwanawe.

Habari hizo za tanzia ya ghafla ya ‘Sasha’ kama alivyofahamika kutokana na filamu ‘SUMU’ iliyokuwa imeonyeshwa katika kituo cha televisheni Kenya K24 imewaacha wengi waliomfahamu na mshangao.

Kando na Sumu, Maureen Wanza waliigiza katika filamu kama vile Almasi kama ‘Stela’ na sasa Kashfa ambayo bado iko jikoni.

VOA imezungumza na Ann Hamburg mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Asheena Pictures ambayo ilikuwa imemwajiri Bi Wanza, na ameelezea masikitiko yao juu ya kumpoteza muigizaji nguli aliyekuwa na nidhamu ya kazi.

“Maureen Wanza alijitolea kazini, alikuwa na nidhamu ya kazi na katika majukumu aliyopewa kwenye filamu alicheza kwa ustadi wa hali ya juu na hii ndio maana tulimhusisha katika filamu tulizotengeneza” alisema Ann Humburg.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook Mwigizaji Kenneth Ambani (Benjami Kido) ambaye yuko Afrika Kusini kushiriki warsha” ameelezea kusiskitishwa na kifo cha Wanza ambaye alikuwa rafiki kando na kuwa waliigizia pamoja katika filamu ya “Sumu.

Oktoba 2015 Maureen Wanza alikuwa ameorodheshwa miongoni mwa waigizaji bora kuwania tuzo la KALASHA kutokana na jukumu lake kwenye filamu ‘SUMU’ .

Amefariki kipindi ambacho nyota yake ya uigijazi ilikua inan’gaa na alitarajiwa kunyakua tunu kadhaa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Liberty Adede, Kenya