Tanzania yaanza sensa ya watu na makazi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Tanzania Jumanne imeanza zoezi la hesabu ya watu na makazi ambalo hufanyika kila baada ya miaka 10 ili kujua idadi kamili ya watu wake.

Zoezi hili limekuwa likihamasishwa kwa kipindi kirefu na kumekuwa na utolewaji elimu wa umuhimu na namna zoezi hilo litakavyofanyika.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliongoza kwa kuonyesha mfano pale alipoandikishwa na familia yake na afisa wa idara ya takwimu ya taifa (NBS) Phausta Ngitigi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Tanzania, zoezi hilo lilichukuwa dakika 30 katika ikulu ya Dodoma, ambapo mkurugenzi mkuu wa NBS aliambatana na kamishna mkuu wa sensa, spika mstaafu wa bunge la Tanzania, Anne Makinda.

Licha ya kwamba Jumanne ilikuwa siku ya mapumziko kupisha zoezi la sensa, kamishna mkuu wa sensa Anne Makinda amesema watu wasiwe na wasiwasi kwani zoezi litaendelea.

Katika mkutano na wanahabari akiwa na maafisa wa idara ya taifa ya takwimu, kamishna mkuu wa sensa Anne Makinda amesema zoezi hilo ni endelevu kwa siku saba zijazo.

Makinda amewataka watu kuwa na subira, na kuwahakikishia kwamba wale ambao hawakupata fursa ya kuhesabiwa Jumanne, bado kuna siku kadhaa zimesalia kukamilisha sensa ya watu na makazi.

Kuelekea kuanza kwa sensa ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2012, watu wanaoishi Tanzania walitakiwa kuandaa taarifa zao muhimu ikijumuisha kitambulisho cha taifa, na nambari za simu ili maafisa wa sensa waweze kuwapigia simu pale wanapo hitaji taarifa zaidi.