Lissu aahidi uhuru kamili wa vyombo vya habari Tanzania

Mgombea urais Tanzania Tundu Lissu wa chama cha Chadema

Asema endapo atachaguliwa kuwa rais kutakuwa na "uhuru kamili" wa vyombo vya habari bila kusimamiwa au kuingiliwa na serikali.

Mgombea urais nchini Tanzania kupitia chama cha upinzani cha Chadema, Tundu Lissu, ameahidi kwamba vyombo vya habari nchini humo vitakuwa na uhuru mkubwa wa kufanya kazi zao endapo atachaguliwa kuwa rais.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Mwanza ambako amekuwa akiendelea na kampeni Jumamosi, Lissu amesema atafuta sheria nyingi za vyombo vya habari ambazo zimekuwa zikiwekwa na awamu kadha za serikali za Tanzania.

Alirudia matamshi yake kwamba endapo atashinda uchaguzi serikali yake itafuta idara ya maelezo ya serikali akidai kuwa ni masalia ya mfumo wa kikoloni.

Lissu amesema mfumo wa sheria za vyombo vya habari Tanzania kwa sasa una lengo la kuwaziba mdomo wanahabari. Utawala wake utakuwa na lengo la kuwafungua mdomo wanahabari, kwa kufuata mfumo wa uhuru wa vyombo vya habari nchini Ghana.

Sheria na kanuni zinazosimamia vyombo vya habari zimefanyiwa mabadiliko na nyingine kuimarishwa zaidi katika utawala wa awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli. Miongoni mwao ni sheria za habari mtandaoni na kuanzishwa kwa leseni za kuendesha mifumo kama blogu au akaunti za Youtube na kadhalika.

Sheria hizo zimetumiwa mara kadha na serikali ya Tanzania kufungia au kupiga faini vyombo vya habari kwa kile serikali inachodhania ni maudhui yanayokiuka sheria na kanuni za habari.

Msimamo wa serikali ya Tanzania ni kwamba sheria na kanuni za vyombo vya habari zinahitajika kuhakikisha uadilifu katika kazi hiyo na pia kulinda maslahi ya taifa. Sheria za mtandaoni pia zina lengo la kulinda maslahi ya watu binafsi baada ya matukio ya watu kudhalilishwa mitandaoni.