Mahakama ya Rufaa Tanzania yaidhinisha marufuku ya ndoa za utotoni

Ndoa za utotoni

Serikali ya Tanzania Jumatano imeshindwa tena katika kesi ya ndoa za utotoni baada ya Mahakama ya Rufaa nchini humo kutupilia mbali pingamizi la serikali liliokuwa likitaka sheria ya ndoa chini ya miaka 18 iendelee.

Serikali ilikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoa ushindi kwa watetezi wa haki za binadamu (Msichana Initiative) waliokuwa wakipinga baadhi ya vipengele vya sheria ya ndoa kwa madai vilikuwa vikimkandamiza mtoto wa kike.

Uamuzi wa mahakama hiyo ya rufaa unakamilisha safari ya miaka mingi ya watetezi wa haki za binadamu wakipigania ustawi wa mtoto wa kike ambao unadaiwa kukandamizwa na sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Katika shauri lao mbele ya mahakama kuu na baadaye mahakama ya rufaa, asasi za kiraia zilidai kitendo cha sheria ya ndoa kutamka kwamba mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 wakati yule wa kiume anaweza kuoa akiwa na umri wa miaka 15, inakandamiza ustawi wa watoto wote na pia inaleta mazingira ya kibaguzi kwa watoto hao jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya nchi.

Mmoja wa mawakili wa upande wa walalamikaji, Alex Mngongolwa amesema, sheria hiyo ya ndoa, siyo tu kwamba ilikuwa inakiuka misingi ya katiba ya nchi, lakini pia ilikuwa haiowani na mikataba mingi ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Wachambuzi wa haki za binadamu wanasema kutenguliwa kwa sheria hiyo kunaweza kukawa ni habari njema kwa mamilioni ya watoto hasa wale walioko maeneo ya vijijini ambako wamekuwa waathirika wakubwa wa ndoa za utotoni.

Ripoti nyingi za tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watoto wengi hushindwa kuendelea na masomo kutokana na ama kulazimishwa kuolewa au kupachikwa mimba kutoka kwa wale wanaojulikana kama ‘mabazazi’ yaani wanaume wenye kupenda kuwarubuni kingo’ono watoto wa kike.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, George Njogopa, Tanzania